Header Ads


NYAMLANI AJITOA KWENYE KINYANG'ANYIRO CHA URAIS TFF

Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athumani Nyamlani amejitoa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Uraisi wa Shirikisho hilo unaotarajia kufanyika Agosti 12, mwaka huu.
 Image result for Athumani Nyamlani
Nyamlani aliwasilisha barua TFF siku ya Jumapili Juni 25, mwaka huu ikiwa ni siku moja tu tangu Kamati ya Uchaguzi ipitishe jina lake kuwa miongoni mwa wagombea 10 wanaowania nafasi hiyo ya urais.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF Sababu iliyotajwa kwa Nyamlani kujitoa katika mbio za kuwania Urais ni masuala binafsi ya Mgombea mwenyewe ambayo hayajawekwa wazi.

Kwa msingi huo, wagombea wanaobaki kwenye kinyang’anyiro ni tisa wakiongozwa na Rais wa sasa, Jamal Malinzi anayetetea nafasi, Imani Madega, Wallace Karia, Fredrick Masolwa, Fredrick Mwakalebela, John Kijumbe, Shija Richard, Ally Mayay na Emmanuel Kimbe.

Idadi ya wagombea mpaka sasa ni 72 baada ya kuondolewa kwa Abdallah Mussa aliyekuwa akiwania nafasi ya kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji TFF kutoka Kanda inayojumuisha Mikoa ya Kagera na Geita kutokana na sababu ya kutoambatanisha kivuli cha cheti chake cha elimu ya sekondari.

Wagombea wote kuanzia nafasi ya Urais hadi ya Ujumbe wanatakiwa kufika kwenye Usaili wa kwanza unaotarajiwa kuanzia Juni 29, mwaka huu.

No comments

Powered by Blogger.